Akiongea na Bongo5, Mabeste ambaye leo ametangaza kutokuwa chini ya label hiyo kupitia Facebook, amesema pamoja na label hiyo na kutengeneza hits nyingi, muziki wake haukuwa ukimpa kipato anachostahili na kusema kuwa tatizo lake na B’Hits ni katika kuufanya muziki wake uingize fedha zaidi pamoja na kuufanyia promotion.
Amesema nyimbo zote alizowahi kutoa amekuwa akiachiwa yeye zaidi kuzifanyia promotion na kuzifikisha mahali kitu ambacho anaamini ilikuwa ni kazi ya label yake.
“Sitaki kuonekana mzigo kwao. Haiwezekani kila siku wao wawe wanarekodi halafu wao hawaoni faida. Baada ya kutoona faida, wanarekodi nyimbo nyingine tena wananipa inaenda,” amesema Mabeste.
Aliongeza kuwa anaumia kuona producer wake Pancho ambaye alimkutanisha na B’Hits miaka mitano iliyopita hapati faida ya muziki wake. Hata hivyo amekanusha madai ya kufanya show bila kutoa taarifa kwa uongozi na kudai kuwa katika dunia ya sasa si rahisi kufanya show kwa siri bila kujulikana.
“Sasa mabadiliko ambayo yanatokea ndani ya haya maisha, wanahisi maybe mimi ninapata show siwaambii. Hivi hii Tanzania sasa hivi social networks ilivyotawala, kuna mahali unaweza kupiga show mtu asijue? Na nani atakuita show yake na aachie kuifanyia promotion kwa social network,” amehoji Mabeste.
Mabeste amesema kutokana na maisha kubadilika na kwakuwa sasa amekuwa baba, kiasi alichokuwa anakipata akiwa B’Hits ni kidogo kuweza kukidhi mahitaji yake ya kila siku na hivyo kumfanya aishi na stress wakati ana uwezo mkubwa.
Hata hivyo CEO wa B’Hits Music Group, Hermy B amesema anashangaa kumsikia Mabeste akilalamika hivyo wakati wao walimtoa mbali ambako alikuwa akiishi maisha ya chini na kuingia gharama nyingi za kumtunza ikiwa ni pamoja na kumlipia kodi ya nyumba, kumnunulia nguo pamoja na kumpa fedha ya kujikimu pale alipokuwa akihitaji.
Hermy B amesema kama akiamua kujumlisha gharama alizotumia kwa Mabeste zinafika si chini ya shilingi milioni 30 na haoni kama Mabeste ana uwezo wa kuzirejesha.
Ameongeza kuwa wote Mabeste, Gosby na Vanessa hawana shukrani kwa kile B’Hits imewafanyia.
Ametoa mfano kuwa video ya Closer ya Vanessa Mdee aligharamikia fedha zake kutoka mfukoni ambazo ni takriban shilingi milioni 8 ambazo hazijawahi kurudi hadi sasa na pia alilipia kwa hela yake hata kazi alizofanya kwenye studio nje ya B’Hits.
Naye Amani Joachim, ambaye ni mwanasheria na mmoja wa viongozi wa B’Hits, alisema Vanessa Mdee na Gosby waliondolewa B’Hits kutokana na kuingia mkataba wa kufanya show ya Fiesta Dar bila kuutaarifu uongozi. Amesema wawili hao walifikia hatua ya kwenda kufanya fujo B’Hits wakidai nyimbo zao kwaajili ya kutumbuiza kwenye show hiyo hali iliyokiuka masharti ya mkataba wao.
Ameongeza kuwa ukimya wao umewafanya watu wengi waamini kuwa wasanii hao walijiondoa wenyewe wakati uongozi ndio ulifanya uamuzi wa kwanza wa kuwaondoa.
Pamoja na hivyo, Hermy B amesema B’Hits itaziachia nyimbo zote za wasanii hao zichezwe redioni kwakuwa kuzifungia kutakuwa na hasara kwao kutokana na kutumia nguvu na akili nyingi kuziandaa.
Hata hivyo amesema, wasanii hao hawatakuwa na haki ya kuzitumia popote kwakuwa ni mali halali ya kampuni. Hermy B amesema, uongozi wa B’Hits hauna ugomvi na wasanii hao na mwanzoni mwa mwaka ujao wanatarajia kutangaza wasanii wapya watakaokuwa chini ya label hiyo.
0 comments:
Post a Comment